| Maelezo: Suuratul Baqara |
| (1) Katika Aya hii ipo sehemu ya kuonesha muujiza wa Qur'ani Tukufu: nayo ni kauli yake Mtukufu "mbingu kama paa". Haya asingeyajua Nabii asiyejua kusoma ila kwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu, nayo ni kuwa mbingu kwa kisayansi ni kila kilicho izunguka dunia pande zote, na kwa ukomo wowote, na kwa sura yoyote katika anga, mpaka huko juu kabisa kwenye sayari nyenginezo, zilizoenea zisio na mwisho. Zote hizo zinazunguka kwa mpango wa ajabu, na sisi tunapata uvukuto na mn'gao wake, nazo zinakwenda kwa nguvu ya mvutano kama smaku. Katika sehemu ya mwanzo ya mbingu iliyo tuzunguka lipo anga linalo tukinga kama paa na mianga inayo dhuru kutokana na hizo sayari. Na tabaka hizo huachilia mianga yenye faida tu, ndipo penye mawingu yaletayo mvua. |
| (1) Aya hii inaonyesha kuwa ahadi, au agano, ni waajibu wa pande zote mbili zilizo ahidiana kutimiza lilio lazimika. Akiacha mmojapo basi haimlazimu wa pili kutimiza agano lake. |
| (1) ("Masiku" ni wingi wa Usiku. Wingi wa siku ni siku, kama ilivyo sahani, sabuni, silaha, sinia, sungura, saa. Ni makosa kwa Kiswahili kusema "masiku" kuwa ni wingi wa siku; "Masiku" ni wingi wa "Usiku". Kutumia "Masaa" kuwa ni wingi wa "Saa" ni makosa.) |
| Kabla ya Uislamu zilikuwapo katika mji wa Madina kabila mbili za Kiarabu ambazo zilikuwa na uadui baina yao, nazo ni Aus na Khazraj. Na pia zilikuwako kabila za Kiyahudi nazo ni Banu Quraidha na Banu Nnadhir. Banu Quraidha walifungamana na Aus, na Banu Nnadhir walifungamana na Khazraj. Ilikuwa kabila mbili za Kiarabu zikipigana, zile kabila za Kiyahudi nazo huingia vitani, kila kabila upande wa rafiki zake, na zikiuwana na wenzao wa dini moja nao, na wakifukuzana makwao. Lakini kila moja katika kabila mbili hizo za Kiyahudi zikishughulika baadaye kuwakomboa mateka walio tekwa na rafiki zao wa Kiarabu. Wakiulizwa kwa nini mnawakomboa na hao walikuwa wakipigana nanyi upande wa maadui zenu? Wao wakisema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tuwakomboe mateka wa Kiyahudi. Na wanajifanya hawajui kama Mwenyezi Mungu amewaamrisha vile vile wasiuwane wala wasitoane majumbani mwao. Kwa hivyo ndio wanaamini sehemu ya Kitabu na wanaikataa nyengine. |
| (1) (Mwenyezi Mungu alimwambia Musa: "Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe...mtu asiye sikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake." |
| (1) Katika lugha ya Kiyahudi ya Kiebrania lipo neno "Rai'nu" ambalo limejengwa na neno "Ra'" kwa maana ya "Shari" na neno "nu" linaonesha jamii, wingi. Na maana ya neno lote ni kuwa "Wewe ni shari yetu", wakikusudia kumwambia Mtume hayo. |
| (1) Wanasema wafasiri kuwa Mayahudi wanaelekea kwenye Mwamba katika Beitul Muqaddas na Wakristo wanaelekea Mashariki. |
| (1) Qurani imeutangulia utibabu wa kisasa kwa kukataza kula mzoga, kwani kifacho kwa ukongwe au ugonjwa husabibishwa na sumu inayo mdhuru mlaji. Kadhaalika cha kunyongwa au maradhi huinajisi damu, na ndani yake huwamo vingi vya kudhuru kama jasho na mkojo. Na nguruwe husabibisha maradhi ya khatari kama TRICHINOSIS ambayo khatimaye huharibu moyo na mapafu na husabibisha mauti. |
| (1) Hali ya dharura inaruhusisha kinacho harimishwa, kwa sababu mauti ya yakini yanashinda madhara yanayo weza kustahamilika, na kwamba mwenye kulazimika kwa dharura haimfalii kupindukia mpaka wa dharura, wala asikiuke kile alicho lazimika kukila. |
| (1)Waarabu zama za jahiliya walikuwa hawafanyi usawa baina ya watukufu na wanyonge. Akiuliwa mwongozi hawatosheki na kumuuwa muuwaji bali huyo huachwa akenda kulipizwa kisasi kwa mwongozi wa kabila ya muuwaji. Kwao roho si sawa, na damu si sawa. Uislamu haukukubali haya, lakini ukapasisha Kisasi, roho kwa roho, mwenye kuuwa huuwawa. Muuwaji yeyote awaye atauliwa akiwa muungwana, mtumwa au mwanamke. Haya ni kwa ajili ya usawa katika damu; hapana mwenye damu tukufu na damu isiyo tukufu. Na inafahamika kwa ishara kuwa nafsi kwa nafsi. Na hii ni sharia ya milele, ilikuwako katika Taurat, na Injil na Qur'ani. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na tuliwaandikia kuwa nafsi kwa nafsi..." (taz. sura Almaida ). Na Mtume s.a.w. amesema: "Damu za Waislamu ni sawa." Na amesema: "Nafsi kwa nafsi". Zingatia: Uislamu kwa sharia ya kisasi ina nadhari nyengine, sio kama kanuni za kutungwa. Imewapa wenye kuuliwa mtu wao haki ya kutaka muuwaji auwawe, kuondoa fitna na umwagaji wa damu mkubwa. Imewapa haki ya kusamehe au kulipwa kisasi, wala haizuilii serikali kumfedhehi aliye uwa ikiona hivyo ni maslaha. Uislamu hauzingatii sababu ya kuuwa, kwani mwenye kuuwa amedhulumu hata ikiwa sababu gani. Na huenda ukitafuta sababu akaonewa huruma mkosa, na kumpuuza mkoswa. Na hayo hupelekea mchafuko wa watu kuchukua kisasi mkononi mwao, na kuzalikana makosa juu ya makosa ya kuuwa, kwa kutoridhika wale walio uliwa mtu wao. Nadharia hii ya Kiislamu sasa inadurusiwa katika vyuo vikuu vya Ulaya. |
| (1) Imethibiti kwa matibabu ya kisasa kuwa Saumu kwa namna ya Qur'ani ina faida nyingi, katika hizo ni kuwa inasaidia katika kutibu maradhi ya sukari, inatengeneza matumbo, inapunguza maumivu ya viungo, na maradhi ya moyo, inapumzisha nyama za mwili, na inasafisha uchafu mwingi wenye madhara, na pia inakuwa ni kinga kwa maradhi mengi mengineyo. Je, vipi kwa mtu asiye jua kusoma na kuandika ayajue yote haya? |
| (1) Uislamu unahisabu mwezi unapo andama na kugeuka sura kwa watu kupimia nyakati za ibada, na pia kwa mambo yao ya kidunia, kwa sababu hayo ni mambo ya kuonekana, na kwa hivyo taarikhi inajuulikana kwa sura ya mwezi. Mwezi kwa hakika ni kama kioo kinacho onyesha mwangaza wa jua huku duniani. Mwezi ukiwa kati baina ya jua na dunia hauonekani, na baadae mwezi mchanga unaandama na wakaazi wa dunia wanajua kuwa mwezi mpya umeanza. Ukifika mwezi katika upande unao kabiliana baina ya jua na dunia ndio unapo kuwa wakati wa mbaamwezi, mwezi mpevu. Khalafu unaendelea kupungua kama ulivyo kuwa kwanza ukizidi kukua. Kwa hivyo taarikhi inaanza tangu pale ulipo kuwa mwezi mchanga. Pale unapo onekana mwezi mchanga kama uzi ndio mwezi umeandama, huonekana upande wa magharibi, hata kwa dakika chache baada ya kuchwa jua nao hupotea. Hivyo hivyo siku baada ya siku huhisabiwa mpaka zipite siku 29 au 30. |
| Aya 190 mpaka 195 zinaeleza sharia ya vita katika Uislamu. Nazo zinaeleza kwa matamshi yalio wazi haya yafuatayo: 1. Ruhusa ya kupigana imetolewa kwa ajili ya kujilinda na uvamizi wa vita wa vitendo khasa, au zikidhihiri dalili kuwa maadui wanataka vita. Vita havikulazimishwa kwa ajili ya vita wala kwa sababu ya kutaka kuwasilimisha watu kwa kuwauwa na kuwapiga vita. 2. Kunakatazwa kuvamia au kuanza uadui kwa njia yoyote ile. Basi hapana ruhusa kufanyiwa uadui asiye pigana, wala hapana ruhusa kuvuka mipaka ya uadui wakati wa vita: basi hauliwi asiye chukua silaha, wala hakhusiani na vita bali ni mwenye kukumbwa tu na vita. Wala hauliwi mwenye kusalimu amri na akatupa silaha. Wala hapana ruhusa kuwavunjia watu nyumba zao, huko ni kupita mpaka. 3. Mzingatie fadhila iliyo onyeshwa kwa kuamrishwa kuchamngu. Basi msivunje heshima ya wanawake kuwanajisi, hata washirikina wakifanya hayo. Wala msiwakatekate walio uwawa hata ikiwa makafiri wakiwafanyia hayo Waumini. Washirikina walimfanyia hayo Bwana wa Mashahidi, Hamza, wala Mtume s.a.w. hakutoa ruhusa kumfanyia hayo maiti yeyote, bali alikataza akasema:"Tahadharini msiwakatekate maiti". 4. Vita vinakwisha wakiacha washirikina kuwafitini Waumini katika Dini yao, na Dini inakuwa inataka akili na nyoyo zimwelekee Mwenyezi Mungu kwa uhuru. 5. Hapana vita katika mwezi mtukufu, nayo ni miezi ya Hija na Umra. Ikiwa washirikina watapigana katika miezi hiyo, basi Waumini nao yawapasa wapigane. 6. Kuacha kutoka kwenda pigana na maadui wanauwa pasina nasi kupigana nao ni kuipoteza kheri na wema. Kwa haya inadhihiri kuwa vita vya Islamu vina fadhila katika sababu zinazo pelekea kuanza kwake, na vina uadilifu katika kuviendesha. Viwapi hivi na vita vya mataifa mengine ya zamani na ya sasa! Vita vyao hao ni vya uchafu, na vita vya Islamu ni vya Haki na vyenye fadhila. > |