Kwa jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Maelezo: Suurat Al-Ah'zab

Utangulizi:

Rudi kwenye sura

* 1. Ewe Nabii endelea hivyo hivyo, kama ulivyo, kumcha Mwenyezi Mungu, wala usiyakubali mawazo ya makafiri na wanaafiki. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa kuvijua, ni Mwenye hikima katika kauli yake na vitendo vyake.
Rudi kwenye sura

* 2. Na fuata wahyi unao teremka juu yako kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anaye kufunulia kwa wahyi anazo khabari hata za mambo madogo madogo unayo yatenda wewe, na wanayo yatenda makafiri na wanaafiki.
Rudi kwenye sura

* 3. Na wewe mwachilie mambo yako yote Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kabisa kuwa ni mtegemewa wa kila jambo.
Rudi kwenye sura

* 4. Mwenyezi Mungu hakumjaalia mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake; wala hakumfanya mke wa yeyote katika nyinyi kuwa ni mama yake, pale anapo sema ati: Wewe kwangu mimi kama mgongo wa mama yangu! Wala hakuwafanya watoto mnao wapanga kuwa ni wenenu, kuwa hakika ni wana wenu kwa nasaba. Hayo ya kuwafanya watoto wa kupanga kuwa ni wenenu, ni kauli inayo toka kwenye vinywa vyenu, wala hayana ukweli. Hapana hukumu yoyote inayo tokana na hayo. Na Mwenyezi Mungu anasema jambo lilio thibiti la hakika. Na anakuongozeni mlifikie. Na Yeye peke yake Subhanahu ndiye anaye ongoa watu kwenye Njia iliyo sawa.
Rudi kwenye sura

* 5. Wanasibishieni hawa watoto kwa baba zao khasa. Hayo ndiyo ya uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikiwa hamwajui baba zao walio nasibiana nao khasa, basi hao ni ndugu zenu katika Dini na rafiki zenu wa kuwanusuru. Wala nyinyi hamna dhambi ikiwa mmewanasibisha na watu wasio kuwa baba zao kwa kukosea. Lakini inakuwa dhambi kwa mlio kusudia kwa nyoyo zenu baada ya kwisha jua yaliyo. Na Mwenyezi Mungu anakusameheni kwa kukosea kwenu, na anaikubali toba yenu kwa makosa mliyo kusudia.
Rudi kwenye sura

* 6. Nabii Muhammad ni mwenye kustahiki zaidi urafiki kwa Waumini, na ana huruma zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Basi yawapasa wao wampende na wamt'ii. Na wake zake ni Mama zao kwa kuwatukuza na kuwahishimu, na kuwa ni haramu juu yao kuwaoa baada yake. Na jamaa walio khusiana ni karibu zaidi kuliko Waumini wenginewe na Wahajiri, walio hama Makka, kwa kurithiana wao kwa wao kama ilivyo wajibika katika Qur'ani. Lakini inafaa kumfanyia wema mlio fanya urafiki naye katika Dini asiye kuwa jamaa yenu, kwa kuwapa wema na mapenzi au hata kumuandikia mali katika wasia. Hayo ya kurithiana jamaa walio khusiana yamethibiti katika Kitabu cha Qur'ani wala hayawezi kubadilishwa.
Rudi kwenye sura

* 7. Na kumbusha pale tulipo fanya agano na Manabii wote walio tangulia kuwa watafikisha ujumbe na wito kulingania Dini iliyo sawa, na wewe, na Nuhu, na Ibrahim, na Musa, na Isa bin Maryamu; na tukachukua kwao agano lenye shani kubwa.
Rudi kwenye sura

* 8. Ili Mwenyezi Mungu awaulize Manabii Siku ya Kiyama juu ya waliyo waambia kaumu zao. Na Yeye amewaandalia wenye kuwakataa Mitume adhabu yenye kutia uchungu.
Rudi kwenye sura

* 9. Enyi mlio amini zikumbukeni neema na fadhila za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu, pale yalipo kujieni makundi katika Siku ya Handaki. Tukawapelekea upepo mkali wa kimbunga ubaridi, na Malaika ambao nyinyi hamwaoni. Kikawaingia kiwewe katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu alikuwa Mwenye kuviona vitendo vyenu, na ukweli wa niya zenu. Basi akaingia kukulindeni.
Rudi kwenye sura

* 10. Walipo kujieni kutoka upande wa juu ya bonde, na kutoka chini, na macho yakakodoka, na nyoyo zikapanda mpaka kwenye koo, kwa kufazaika na kubabaika. Na nyinyi katika wakati ule wa shida kubwa kila namna ya dhana zilikujieni juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu. Si makusudio ya maneno haya kuwa maadui walikuja kutoka kila upande. Tukiangalia ufafanuzi wa tukio hili inadhihirika kuwa makusudio ni kuwa walio kuja kutoka upande wa juu ya Waislamu, ni kabila ya Ghat'fan na walio wafuata katika wakaazi wa Najdi, kwani wao walikuja pande za juu ya Bara Arabu upande wa mashariki. Na inatudhihirikia kuwa walio kuja upande wa chini ya Waumini ni Makureshi, kwa sababu wao walikuja kutoka upande wa chini ya Bara Arabu upande wa magharibi.
Rudi kwenye sura

* 11. Katika wakati ule Waumini walifanyiwa mtihani juu ya kusubiri kwao juu ya Imani. Wakatikisika kwa khofu kwa mtikiso mkubwa.
Rudi kwenye sura

* 12. Na kumbuka shaka iliyo waingia wanaafiki na wagonjwa wa nyoyo walipo sema: Ahadi aliyo tupa Mwenyezi Mungu na Mtume ni ahadi ya uwongo, imekusudiwa kutudanganya tu.
Rudi kwenye sura

* 13. Na kumbuka walipo sema kikundi cha wanaafiki na ambao wanao rega rega: Enyi watu wa (Yathrib, yaani) Madina! Hapana maana kubakia hapa nyinyi katika vita hivi vya kushindwa. Rudini mwende makwenu. Na kundi jingine kati yao walimtaka ruhusa Mtume warejee Madina, na wakasema: Hakika nyumba zetu hazina ulinzi. Hatuna budi kurejea tukazilinde. Wala nyumba zao hazikuwa khatarini kabisa kama walivyo sema. Hawakutaka ila kukimbia vita tu, kwa udhuru wa uwongo.
Rudi kwenye sura

* 14. Lau kuwa makundi ya majeshi ya maadui wangeli waingilia Madina kwa kila upande, na wakawataka watangaze kuwa wameuwacha Uislamu na wawapige vita Waislamu bila ya shaka wangeli wakubalia yale waliyo takiwa, na wala wasingeli sita ila muda mfupi tu.
Rudi kwenye sura

* 15. Na hakika hawa wenye kukimbia kutoka midani ya vita walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kuwa watasimama imara katika vita pamoja na Mtume, na wala hawatakimbia. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa kwa yule mwenye kuitoa, na yampasa aitimize.
Rudi kwenye sura

* 16. Waambie: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa ndio mnayakimbia mauti au kuuwawa, maadamu ajali yenu imekwisha fika. Na ikiwa haijafika, basi hamtobaki mkistarehe katika dunia ila kwa muda wa umri wenu, nao ni mchache.
Rudi kwenye sura

* 17. Waambie hawa wanao babaika: Nani atakaye kulindeni na Mwenyezi Mungu akitaka kukuleteeni shari, au atakaye kuzuieni msipate kheri, akitaka Yeye kukurehemuni? Wala hawatapata badala ya Mwenyezi Mungu yeyote wa kuwalinda au kuwaokoa.
Rudi kwenye sura

* 18. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua wanao zuilia miongoni mwenu, na wanao waambia ndugu zao: Unganeni nasi! Wala hawaingii katika vita vinapo shitadi ila kidogo tu.
Rudi kwenye sura

* 19. Wana pupa juu yenu kwa kuonekana dhaahiri inapo kuwa hapana khofu. Na ikija khofu ya adui au ya Mtume s.a.w. utawaona wanakuangalia na macho yao yanawazunguka hawajitambui, kama hali ya mwenye kuzimia wakati wa sumbuko la kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanapita mpaka kukutukaneni na kukushutumuni kwa ndimi za kukata. Hao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini kwa nyoyo zao, ijapo kuwa wametangaza kuwa ni Waislamu. Basi Mwenyezi Mungu amezibat'ilisha a'mali zao kwa ukafiri wao walio dhamiria. Na kubat'ilisha huko ni jambo jepesi kwa Mwenyezi Mungu. Aya hii tukufu inaashiria ukweli wa kisayansi ambao ulikuwa haukujuulikana namna yake wakati wa kuteremka Qur'ani Tukufu. Ukweli huo ni kuwa jicho wakati wa kukurubia mauti au wakati wa khofu huzunguka. Na katika sababu za hayo ni kuwa kwa shida ya khofu utambuzi hutoweka, ikawa mtu hajitambui. Vituo vya navo zisio tambua katika ubongo hupoteza mizani yake, basi huwa huyo mwenye khofu kama mfano wa mwenye kuzimia kwa kukaribia kufa, jicho lake huzunguka na mboni ya jicho hupanuka, na hubaki katika hali ya kukodoa macho mpaka kufa.
Rudi kwenye sura

* 20. Wanadhani hawa wanaafiki kwamba majeshi ya makafiri yaliyo ungana bado yapo mahali pao wanaizinga Madina. Na hayo makundi ya maadui yakirejea tena, watatamani hao woga laiti wangeli kuwa wanaishi pamoja na mabedui huko majangwani wakidondoa khabari zenu. Na lau wakibaki kwenye kambi zao, na wasikimbie, na majeshi mawili yakapambana, basi hata hivyo wasinge pigana pamoja nanyi ila kidogo tu, kama kujionyesha na watajwe kuwa nao walikuwamo.
Rudi kwenye sura

* 21. Hakika nyinyi mna kiigizo kizuri kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kutaraji rehema ya Mwenyezi Mungu, na neema za Siku ya Mwisho, na akamkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi katika khofu na kutumai, na katika shida, na katika neema.
Rudi kwenye sura

* 22. Na Waumini walipo yaona makundi ya washirikina walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake zamani. Kwani walituahidi tutapata shida, na kisha tutapata ushindi. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Taabu hizi basi, hazikuwazidishia ila nguvu za kumuamini Mwenyezi Mungu, na uzuri wa kuinyenyekea kwao hukumu yake.
Rudi kwenye sura

* 23. Miongoni mwa hawa Waumini wapo watu walio muahidi Mwenyezi Mungu kuwa watasimama imara na Mtume katika vita. Nao wakatimiza ahadi yao. Miongoni mwao wapo walio pata utukufu wa kufa mashahidi, na wengine wamebakia wahai wakingojea nao kupata utukufu huo. Wala hawakuigeuza ahadi ya Mwenyezi Mungu waliyo jikatia juu ya nafsi yao, wala hawakugeuza chochote katika hayo.
Rudi kwenye sura

* 24. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwalipa Waumini walio wakweli kwa sababu ya ukweli wao katika Imani yao na kutimiza kwao ahadi waliyo itoa. Na awaadhibu wanaafiki - pindi akitaka - au amwezeshe aliye elekea, kufikia toba. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe kwa kukubali toba, Mwenye kurehemu kwa kusamehe maasi.
Rudi kwenye sura

* 25. Mwenyezi Mungu akawarudisha nyuma makafiri walio jiunga makundi kumpiga Mtume na nyoyo zao zimejaa chuki. Hawakupata kheri yoyote kwa ushindi wala ngawira. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini wasipate mashaka, kwa kuwapatiliza wale makafiri kwa upepo na Malaika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza wa kutimiliza alitakalo, ni Mwenye nguvu hapana wa kumshinda.
Rudi kwenye sura

* 26. Na Mwenyezi Mungu aliwateremsha walio wasaidia makundi ya maadui katika Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa Bani Quraidha, kutokana na ngome zao walipo kuwa wakijilinda ndani yake. Na akaingiza katika nyoyo zao kitisho. Wengine mkawa mnawawauwa, nao ni wanaume, na wengine mnawachukua mateka, nao ni wanawake na watoto.
Rudi kwenye sura

* 27. Na akakurithisheni ardhi zao, na nyumba zao, na mali zao, na ardhi ambazo nyayo zenu hazijapata kuzikanyaga kabla yake. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Muweza wa kutimiza kila alitakalo.
Rudi kwenye sura

* 28. Ewe Nabii! Waambie wake zako kwa kuwanasihi: Ikiwa mnataka maisha ya duniani na starehe zake, basi jongeeni nitakupeni cha kupunguza upweke wa talaka, itakuwa ni tunza yenu. Na nitakupeni talaka isiyo na uovu ndani yake.
Rudi kwenye sura

* 29. Na ikiwa mnakhiari mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na neema za nyumba ya Akhera, na mnaridhi maisha magumu mlio nayo hivi sasa, basi hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia mfano wenu nyinyi miongoni mwa wanawake walio wema kwa vitendo vyao, ujira ambao haukadiriki.
Rudi kwenye sura

* 30. Enyi wake wa Nabii! Miongoni mwenu mwenye kufanya makosa yaliyo dhaahiri ubaya wake, basi juu ya adhabu yake zinaongezwa adhabu mbili, ili iwe adhabu tatu kwa kulinganisha na mwenziwe. Na kuongeza huko kwa Mwenyezi Mungu ni kwepesi.
Rudi kwenye sura

* 31. Na katika nyinyi mwenye kudumu juu ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, Mwenyezi Mungu atampa ujira mara mbili. Na tumemuandalia kwa Akhera riziki ya kipimo kizuri.
Rudi kwenye sura

* 32. Enyi wake wa Mtume! Nyinyi si kama wanawake wengine kwa fadhila na utukufu. Kama mnataka uchamngu, basi msizungumze kwa maneno ya kuregeza sauti, hata ambaye ana uharibifu katika moyo wake akaingia tamaa. Kusema kwenu kuwe kama kawaida sio kujitia.
Rudi kwenye sura

* 33. Na kaeni nyumbani kwenu, wala msitoke ila kwa haja. Wala msidhihirishe uzuri wenu na mapambo yenu kwa wanaume pale mnapo toka, kama walivyo kuwa wakifanya watu wa ujahili wa zamani. Na timizeni Sala kwa ukamilifu, na toeni Zaka, na fuateni amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka, kwa yote anayo kuamrisheni na kukukatazeni, mpate utukufu na hishima, ili muondokewe na madhambi na maasia, enyi Ahli Baiti Nnabii, Watu wa Nyumba ya Nabii, na akusafisheni kwa usafi usio kuwa na shaka.
Rudi kwenye sura

* 34. Na hifadhini yanayo somwa katika nyumba zenu ya Qur'ani aliyo iteremsha Mwenyezi Mungu, na hikima zilio sawa za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua mambo yalio zama ndani kabisa na ya hakika yake. Basi tahadharini na kwenda kinyume naye na kumuasi Mtume wake.
Rudi kwenye sura

* 35. Hakika wenye kut'ii miongoni mwa wanaume na wanawake, na wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wanaume na wanawake, na wenye kusimama kwa ut'iifu wanaume na wanawake, na walio wa kweli katika kauli zao na vitendo vyao katika wanaume na wanawake, na wenye kusubiri katika kubeba mashaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanaume na wanawake, na wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu wanaume na wanawake, na wenye kuzihifadhi tupu zao kwa yasiyo kuwa halali wanaume na wanawake, na wenye kumdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi katika nyoyo zao na ndimi zao wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia kuwasamehe madhambi yao, na kuwalipa malipo makubwa kwa vitendo vyao.
Rudi kwenye sura

* 36. Haimjuzii Muumini, mwanamume au mwanamke, kuwa na khiari katika jambo lolote baada ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakisha lihukumia. Na mwenye kwenda kinyume na alivyo hukumu Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi amejitenga mbali na njia iliyo sawa kwa umbali ulio dhaahiri.
Rudi kwenye sura

* 37. Na kumbuka pale ulipo mwambia Zaid bin Haritha, ambaye Mwenyezi Mungu amemneemesha kwa kumwongoa kwenye Uislamu, na wewe ukamneemesha kwa kumlea na kumkomboa utumwani: Shikamana na mkeo, Zainab binti Jahsh, na umche Mwenyezi Mungu, na vumilia kukaa naye. Na wewe ulikuwa unaficha nafsini mwako ambayo Mwenyezi Mungu atakuja yadhihirisha, yaani kuwa yeye atampa t'alaka na wewe utakuja muwoa. Nawe ukakhofu watu wasije kukulaumu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye stahiki umkhofu, ijapo kuwa hayo ni mashaka juu yako. Basi Zaid alipo kwisha haja naye, na akampa t'alaka kujiondolea dhiki ya kuishi naye, tukakuoza wewe, ili iwe ni chanzo cha kuvunja ada iliyo mbovu. Baada ya hayo hapana ubaya tena kwa Waislamu kuwaoa walio kuwa wake za walio kuwa wamewapanga utoto, baada ya kwisha wat'aliki. Na amri ya Mwenyezi Mungu aitakayo ni lazima iwe bila ya pingamizi.
Rudi kwenye sura

* 38. Nabii hana makosa kutenda kitendo alicho muamrisha Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ameweka mwendo huo kwa Manabii walio tangulia, kuwa wasipige marfuku alicho wahalalishia na akawakunjulia. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kupitisha alicho pitisha, na hukumu iliyo thibiti.
Rudi kwenye sura

* 39. Manabii hao ndio walio wafikishia watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu kama tulivyo wateremshia. Nao wanamkhofu Yeye, wala hawamkhofu yeyote asiye kuwa Yeye. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Yeye ndiye Muangalizi Mwenye kuhisabu.
Rudi kwenye sura

* 40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu hata iwe ni haramu kwake kumwoa mt'alaka wake. Lakini yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni Mwenye kukhitimisha Manabii wote. Juu yake ni kufikilisha ujumbe kama alivyo muamrisha Mola wake Mlezi, bila ya kumchelea yeyote. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye sura

* 41,42. Enyi ambao mmeamini! Msifuni Mwenyezi Mungu kwa namna mbali mbali za sifa, na mfanye hayo kwa wingi. Na mtakaseni na kila kisicho kuwa laiki naye mwanzo wa mchana na mwisho wake.
Rudi kwenye sura

* 41,42. Enyi ambao mmeamini! Msifuni Mwenyezi Mungu kwa namna mbali mbali za sifa, na mfanye hayo kwa wingi. Na mtakaseni na kila kisicho kuwa laiki naye mwanzo wa mchana na mwisho wake.
Rudi kwenye sura

* 43. Na Yeye ndiye aliye kuahidini kukupeni rehema yake na upole wake. Na Malaika wake wanakuombeeni maghfira na uwongofu, ili Mwenyezi Mungu akutoeni kwenye giza la ukafiri na upotovu, mwendee kwenye nuru na ut'iifu. Na Mwenyezi Mungu hakika ni Mkuu wa kuwarehemu Waumini.
Rudi kwenye sura

* 44. Maamkio yao siku watakapo kutana naye ni: Amani na Salama kwao. Na amewatengezea kwa vitendo vyao ujira wa ukarimu utakao waonyesha fadhila zake.
Rudi kwenye sura

* 45. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma kwa watu wote uwapelekee ujumbe wa Uislamu. Ushuhudie Haki, na uwabashirie Waumini kwamba watapata kheri na thawabu, na uwaonye makafiri kuwa watapata mwisho muovu.
Rudi kwenye sura

* 46. Na umetumwa uwe ni mwenye kuwaita viumbe vyote vimwendee Mwenyezi Mungu kwa amri yake. Na uwe ni taa ya uwongofu kuwaongoa kwa nuru yake waliopo katika kiza cha shaka.
Rudi kwenye sura

* 47. Na wabashirie Waumini kwamba watapata kheri kubwa ya kuzidi katika dunia na Akhera.
Rudi kwenye sura

* 48. Na wala usiwafuate makafiri na wanaafiki, wala usijishughulishe na maudhi yao. Na mfanye Mwenyezi Mungu ndiye Wakili wako wa kumtegemea kukulinda na madhara yao na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakutosha kabisa kuwa ndiye Mtegemewa wa kukukifia na kukukinaisha.
Rudi kwenye sura

* 49. Enyi mlio amini! Mkifunga ndoa na wanawake Waumini, kisha mkawat'aliki kabla ya hamjawaingilia, basi haiwalazimu eda wao mkawa mnaihisabu. Basi wapeni kitu katika mali kwa kuwapoza. Na mwatoe majumbani kwenu bila ya kuwaletea madhara yoyote.
Rudi kwenye sura

* 50. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari. Na tumekuhalishia wajakazi ulio wamiliki mkono wako wa kulia, katika alio kuneemeshea Mwenyezi Mungu. Na tumekuhalalishia kuwaoa mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada, yaani ndugu wa kike, wa mama yako, walio hama nawe. Na tumekuhalalishia mwanamke Muumini akijitolea nafsi yake bila ya mahari, nawe ikawa unataka kumwoa na umempenda. Kujitolea huku ni kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Kwao haifai hivyo. Tunajua hukumu tulizo wafaridhia Waumini kwa wake zao na wajakazi wao, na tuliyo kuruhusu wewe, si wao, ili isiwe dhiki juu yako kwa tuliyo kuhukumia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe madhambi ya waja wake, Mwenye kuwarehemu kwa ukunjufu.
Rudi kwenye sura

* 51. Unaweza kumuakhirisha umtakaye katika kugawa zamu, na ukamjongeza umtakaye. Na kumtaka uliye muakhirisha zamu yake hapana lawama juu yako. Hivyo kuachiliwa utakavyo wewe yakaribia zaidi kupelekea furaha yao na baada ya kuwahuzunikia, na wao wote wawe radhi kwa ulio wapa. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo ndani ya nyoyo zenu, ya kuudhika au kuridhika kwa aliyo kufanyieni sharia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani, Mpole hafanyi papara kuadhibu.
Rudi kwenye sura

* 52. Hawakuhalalikii wanawake wengine baada ya hawa, wala kuwapa t'alaka kwa ajili ya kuwabadilisha kwa wengine uwatakao, hata wakikupendeza kwa uzuri wao. Lakini Mwenyezi Mungu amekuhalalishia wajakazi ulio wamiliki kwa mkono wako. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu, na anakihifadhi.
Rudi kwenye sura

* 53. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila kwa idhini yake kwa ajili ya kwenda kula chakula, bila ya kwenda kungoja wakati mpaka kitapo kuwa tayari. Lakini Mtume akikuiteni, basi ingieni. Na mkisha kula ondokeni. Wala msikae baada yake mkijizoeza mazungumzo nyinyi kwa nyinyi. Kwani hakika kuingia bila ya idhini yake, na kukaa muda mrefu baada ya kwisha kula, kunamuudhi Nabii, naye anakustahini hawezi kukutakeni mtoke. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu hana la kumzuia asiitangaze haki kama wanavyo zuilikana viumbe. Na mtakapo wauliza wake za Nabii s.a.w. haja yoyote, basi waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ni usafi bora kwa nyoyo zenu na nyoyo zao zisiingiwe na uchochezi wa Shetani. Na haikufaliini nyinyi kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake milele, kwa sababu ya hishima yake na yao. Hakika jambo hilo ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Yanarejea maelezo ya ki-ilimu juu ya Aya mbili 58, na 59 za Surat An-nur, katika yaliyo khusu adabu za kuzuru.
Rudi kwenye sura

* 54. Mkidhihirisha walau kidogo katika mambo yanayo muudhi, au mkikificha katika vifua vyenu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Rudi kwenye sura

* 55. Hapana dhambi kwa wakeze Nabii wakitojificha kwa baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au watoto wa ndugu zao wa kiume, au watoto wa ndugu zao wa kike, au wanawake Waumini wenginewe, au watumwa walio wamiliki, kwa sababu ya shida ya kuwahitajia kwa matumishi. Nanyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo aliyo kuamrisheni, wala msipindukie mipaka yake. Kwani Yeye hakika anajua kila kitu, hapana kilicho fichikana kwake.
Rudi kwenye sura

* 56. Hakika Mwenyezi Mungu anamrehemu Nabii wake na yu radhi naye. Na Malaika wanamwombea yeye. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu.
Rudi kwenye sura

* 57. Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuwapinga na kuchochea watu wawakatae, Mwenyezi Mungu amewafukuza kwenye rehema yake duniani na Akhera; na amewaandalia adhabu itayo wavunja kiburi chao.
Rudi kwenye sura

* 58. Na wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake kwa maneno au vitendo, bila ya wao kufanya makosa yoyote, hao basi wamebeba migongoni mwao mzigo wa ule uwongo wao, na inakuwa wametenda dhambi iliyo dhaahiri ubaya wake.
Rudi kwenye sura

* 59. Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake wa Waumini, wateremshe nguo zao juu ya miili yao. Na wakivaa namna hii ni afadhali na wanaelekea zaidi kujuulikana na kwa hivyo wasipate kuudhiwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kumrehemu mwenye kuacha madhambi yake.
Rudi kwenye sura

* 60. Ninaapa! Ikiwa hawataacha hao wanaafiki, na wenye maradhi katika nyoyo zao, na wanao eneza khabari za uwongo katika Madina, hapana shaka nitakusalitisha juu yao, kisha hawatabakia kuwa karibu yako ila kwa muda mchache tu.
Rudi kwenye sura

* 61. Hao wanastahiki laana na kufukuzwa. Kila watapo patikana wakamatwe na wauliwe moja kwa moja.
Rudi kwenye sura

* 62. Mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tangu zamani, kwa walio kuwa wakiwafanyia unaafiki Manabii na Mitume, na wakiasi, ni kuwa huuwawa kila wanapo kutikana. Wala mwendo wa Mwenyezi Mungu haugeuki.
Rudi kwenye sura

* 63. Watu wanakuuliza lini itasimama Saa ya Kiyama. Waambie hao: Hakika ujuzi wa wakati wake uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na nini kitakujuvya? Pengine wakati wa kusimama Saa ya kiyama upo karibu.
Rudi kwenye sura

* 64. Hakika Mwenyezi Mungu amewafukuza makafiri kwenye rehema yake, na amewatengenezea Moto mkali mno.
Rudi kwenye sura

* 65. Hawatatoka humo kabisa. Hawatampata wa kuchukua dhamana ya kuwahami, wala wa kuwatetea.
Rudi kwenye sura

* 66. Siku zitakapo geuka nyuso zao Motoni kutoka hali hii kwendea hali hiyo, wakisema kwa majuto: Laiti kuwa sisi tulimt'ii Mwenyezi Mungu na tungeli mt'ii Mtume!
Rudi kwenye sura

* 67. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwafuata maraisi wetu, na wakubwa wetu katika kukukataa Wewe na Mtume wako. Na wao ndio wakatutenganisha mbali na Njia Iliyo Nyooka.
Rudi kwenye sura

* 68. Mola wetu Mlezi! Wajaalie adhabu yao iwe mardufu, na uwafukuze kwenye rehema yako kabisa kwa kadri ya madhambi yao na makosa yao.
Rudi kwenye sura

* 69. Enyi mlio amini! Msimuudhi Nabii kwa namna yoyote ya udhia, kama wale walio muudhi Musa katika kaumu yake. Na Mwenyezi Mungu akamtoa makosani na akamsafisha na hayo waliyo mzulia. Na Musa mbele ya Mwenyezi Mungu alikuwa ni bwana mwenye hadhi.
Rudi kwenye sura

* 70. Enyi mlio amini! Iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu mkimuasi, na semeni maneno yalio simama sawa yasio kwenda upogo.
Rudi kwenye sura

* 71. Apate kukuwezesheni kutenda mema, na azifute dhambi zenu. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo amepata kufuzu kukubwa kwa kuepuka adhabu, na kupata thawabu.
Rudi kwenye sura

* 72. Sisi kwa hakika tulizitaka mbingu na ardhi na milima zichukue dhamana, nazo zikakataa kuichukua, na wakaiogopa. Lakini mwanaadamu aliichukua. Hakika yeye amekuwa ni mkubwa wa kujidhulumu nafsi yake kwa kutojua jukumu la kuchukua huko.
Rudi kwenye sura

* 73. Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na Mwenyezi Mungu apate kukubali toba za Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwingi wa rehema.
Rudi kwenye sura

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani