Ghaafir Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili
40.Suuratul Ghaafir

Imeshuka Makka Ina aya 85
Orodha ya Sura Faharasa

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0


1. H'a, Mim. 1


2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye kujua. 2


3. Anaye samehe dhambi na anaye pokea toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu, hakuna mungu ila Yeye; marejeo ni kwake. 3


4. Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu ila walio kufuru; basi kusikughuri wewe kutanga tanga kwao katika nchi. 4


5. Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na makundi mengine baada yao. Na kila taifa lilikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate. Na walibishana kwa upotovu ili kuipindua haki. Kwa hivyo niliwakamata. Basi ilikuwaje adhabu yangu! 5


6. Namna hivi limewathibitikia makafiri neno la Mola wako Mlezi ya kwamba wao ni watu wa Motoni. 6


7. Wale wanao beba A'rshi, na wanao izunguka, wanamsabihi na kumhimidi Mola wao Mlezi, na wanamuamini, na wanawaombea msamaha walio amini kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe walio tubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Jahannamu. 7


8. Mola wetu Mlezi! Na waingize katika Bustani za Milele ulizo waahidi. Na uwape haya pia wale walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 8


9. Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye maovu siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa. 9


10. Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya shaka kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu, mlipo kuwa mnaitwa kwenye Imani nanyi mkakataa. 10


11. Watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufisha mara mbili, na umetuhuisha mara mbili! Basi tunakiri madhambi yetu. Basi je, ipo njia ya kutoka? 11


12. Hayo ni hivyo kwa sababu mlikuwa akiombwa Mwenyezi Mungu peke yake mnakataa. Na akishirikishwa mnaamini. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Mkuu. 12


13. Yeye ndiye anaye kuonyesheni Ishara zake, na anakuteremshieni kutoka mbinguni riziki. Na hapana anaye kumbuka ila anaye rejea. 13


14. Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, na wangachukia makafiri. 14


15. Yeye ndiye Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A'rshi. Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa Siku ya Mkutano. 15


16. Siku watakayo dhihiri wao. Hapana kitacho fichikana chochote chao kwa Mwenyezi Mungu. Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Mwenyezi Mungu Mmoja Mtenda nguvu. 16


17. Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo chuma. Hapana dhulma leo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. 17


18. Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa. 18


19. (Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo ficha vifua. 19


20. Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao wanao waomba badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia Mwenye kuona. 20


21. Kwani hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Hao walikuwa wamewazidi hawa kwa nguvu na athari katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwatia mkononi kwa sababu ya madhambi yao. Na wala hapakuwa wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu. 21


22. Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyezi Mungu akawakamata. Bila ya shaka Yeye ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu. 22


23. Na kwa yakini tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi, 23


24. Kumwendea Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo mkubwa. 24


25. Basi alipo waletea Haki inayo toka kwetu, walisema: Waueni watoto wanaume wa wale walio muamini na wawacheni hai wanawake wao. Na haviwi vitimbi vya makafiri ila katika upotovu. 25


26. Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola wake Mlezi! Mimi nachelea asije kubadilishieni dini yenu, au akatangaza uharibifu katika nchi. 26


27. Na Musa akasema: Mimi najikinga kwa Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi anilinde na kila mwenye jeuri asiye iamini Siku ya Hisabu. 27


28. Na akasema mtu mmoja Muumini, aliye kuwa mmoja katika watu wa Firauni aliye ficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu? Na hali naye amekujieni na hoja zilizo wazi? Na akiwa yeye mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, na akiwa mkweli yatakufikieni baadhi ya hayo anayo kuahidini. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa. 28


29. Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni nani atakaye nisaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia? Firauni akasema: Sikupeni shauri ila ile niliyo iona, wala sikuongozeni ila kwenye njia ya uwongofu. 29


30. Na akasema yule aliye amini: Enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni mfano wa siku za makundi, 30


31. Mfano wa hali ya watu wa Nuhu na A'di na Thamudi na wale wa baada yao. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja. 31


32. Na enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni Siku ya mayowe. 32


33. Siku mtakapo geuka kurudi nyuma. Hamtakuwa na wa kukulindeni kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi huyo hana wa kumwongoa. 33


34. Na alikwisha wajieni Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyo kuleteeni; mpaka alipo kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta kabisa Mtume baada yake. Kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha kupotea anaye pindukia mipaka katika maasi anaye jitia shaka. 34


35. Hao ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu pasipo ushahidi wowote ulio wafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walio amini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo muhuri juu ya kila moyo wa jeuri anaye jivuna. 35


36. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia, 36


37. Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyo pambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu. 37


38. Na yule aliye amini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia ya uwongozi mwema. 38


39. Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima. 39


40. Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu. 40


41. Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye uwokofu, nanyi mnaniita kwenye Moto? 41


42. Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule ambaye simjui, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu Mwenye kusamehe? 42


43. Bila ya shaka mnaye niitia kumuabudu hastahiki wito duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanao pindukia mipaka ndio watu wa Motoni! 43


44. Basi mtayakumbuka ninayo kuambieni. Nami namkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake. 44


45. Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizo zifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni. 45


46. Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapo fika Saa ya Kiyama patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa! 46


47. Na watapo hojiana huko Motoni, wanyonge watawaambia walio jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, hamtuondolei sehemu ya huu Moto? 47


48. Watasema walio jitukuza: Hakika sote sisi tumo humo humo! Kwani Mwenyezi Mungu kesha hukumu baina ya waja! 48


49. Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu: Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu. 49


50. Nao watasema: Je! Hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu kwa hoja zilio wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya makafiri hayawi ila ni kupotea bure. 50


51. Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi, 51


52. Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makaazi mabaya kabisa. 52


53. Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na tukawarithisha Wana wa Israili Kitabu, 53


54. Ambacho ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili. 54


55. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na asubuhi. 55


56. Hakika hao wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya uthibitisho wowote uliyo wajia, hawana vifuani mwao ila kutaka ukubwa tu, na wala huo hawaufikilii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. 56


57. Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui. 57


58. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani; na walio amini na watendao mema hawalingani na muovu. Ni machache mnayo yakumbuka. 58


59. Hakika Saa (ya Kiyama) itafika, nayo haina shaka. Lakini watu wengi hawaamini. 59


60. Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike. 60


61. Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni usiku ili mpate kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru. 61


62. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa kila kitu. Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi? 62


63. Namna hivi ndivyo walivyo geuzwa walio kuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. 63


64. Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni ardhi kuwa ni pahala pa kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. 64


65. Yeye ndiye aliye Hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi muabuduni Yeye mkimsafishia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. 65


66. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja zilizo dhaahiri kutokana na Mola wangu Mlezi. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote. 66


67. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanao kufa kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate kufahamu. 67


68. Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa. 68


69. Je! Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu? Wanageuziwa wapi? 69


70. Ambao wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma Mitume wetu. Basi watakuja jua. 70


71. Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa 71


72. Katika maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni, 72


73. Tena wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwashirikisha. 73


74. Badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia makafiri wapotelee mbali. 74


75. Haya ni kwa sababu mlikuwa mkijitapa katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua. 75


76. Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo milele. Basi ni maovu yaliyoje makaazi ya wanao takabari! 76


77. Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu. 77


78. Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa Haki, na hapo wapotofu watakhasiri. 78


79. Mwenyezi Mungu aliye kujaalieni nyama hoa, mifugo, ili muwapande baadhi yao, na muwale baadhi yao. 79


80. Na katika hao mnayo manufaa kadhaa wa kadhaa, na mnapata kwao haja ziliomo vifuani mwenu; na mnachukuliwa juu yao, na juu ya marikebu. 80


81. Naye anakuonyesheni Ishara zake. Basi Ishara gani za Mwenyezi Mungu mnazo zikataa? 81


82. Kwani hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa walio kuwa kabla yao? Wao walikuwa wengi kuliko hawa, na wamewashinda kwa nguvu na athari katika nchi. Wala hayakuwafaa hayo waliyo kuwa wakiyachuma. 82


83. Walipo wajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi walijitapa kwa ilimu waliyo kuwa nayo. Basi yakawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara. 83


84. Walipo iona adhabu yetu walisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni wa pekee, na tunaikataa miungu tuliyo kuwa tukiishirikisha naye. 84


85. Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa kitu wakati ambao wamekwisha iona adhabu yetu. Huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kuwa kwa waja wake. Na hapo walio kufuru walikhasiri. 85


Sura Nyingine Faharasa

Chagua Sura Nyingine:

Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com 
Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani